Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Mbamba-Bay mara baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango kumpatia fursa ya kuzungumza na wananchi wa eneo hilo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.
Deogratius Ndejembi amesema wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Mbiga
watanufaika na ujenzi pamoja na ukarabati barabara unaofanywa na
Serikali kupitia fedha za Mradi wa Uboreshaji Miundombinu katika Miji
(TACTIC), AGRI-CONNECT na zilizotengwa kwenye bajeti ya TARURA.
Mhe. Ndejembi amesema hayo akiwa katika Halmashauri ya Mji Mbinga,
mara baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango kumpatia fursa ya kuzungumza na wananchi
wa Mbinga.
Mhe. Ndejembi amesema, kupitia mradi wa TACTIC usanifu wa kujenga
barabara za lami 12 katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga utakamilika
muda si mrefu na mkandarasi ataanza ujenzi, na kuongeza kuwa kupitia
mradi huo Mbinga itajengewa soko la kisasa.
Mhe. Ndejembi ameainisha kuwa, kupitia mradi wa AGRI-CONNECT
barababara nyingine ya Luwaita yenye urefu wa kilomita 15.7 ambayo
usanifu wake umeshakamilika, imewekwa kwenye mpango wa kujengwa
kwa kiwango cha lami katika mwaka huu wa fedha 2023/24.
Aidha, Mhe. Ndejembi amesema, ipo barabara inayotoka Mbinga kwenda
Mpepai na Liparamba yenye urefu wa Kilomita 41.87 ambayo imetengewa
milioni 400 katika mwaka huu wa fedha 2023/24 kwa ajili ya kutengeneza
maeneo korofi ili iweze kutumika wakati wote.
“Mhe. Makamu wa Rais, ninawahakikishia wananchi wa Mbiga kuwa Mhe.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yuko kazini kuwaboreshea miundombinu
ya barabara ambayo ni chachu ya maendeleo katika taifa,” Mhe. Ndejembi
amesisitiza.
Sanjari na hilo, Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa ndani kipindi cha mwaka
mmoja wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita, bajeti ya TARURA kwa
ajili ya ujenzi wa barabara katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga iliongezwa
kutoka milioni 930 hadi bilioni 2.2, na katika mwaka huu wa fedha TARURA
imetengewa zaidi ya bilioni 2.9 kwa ajili ya ukarabati wa barabara zilizopo
katika halmashauri hiyo ya mji.