Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema kuwa Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imejipanga kuhakikisha inarejesha mawasiliano ya barabara zote na madaraja yanayoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha ndani ya muda mfupi pindi yanapoharibiwa.
Aidha, Bashungwa amewaelekeza Mameneja wa TANROADS Mikoa yote kuendelea kufanya ukaguzi wa madaraja na makalvati pamoja na kuondoa matope na takataka ambapo ametaka zoezi hilo kuwa endelevu.
Bashungwa ametoa agizo hilo Aprili 28, 2024, Mkuranga Mkoani Pwani wakati akikagua zoezi la urejeshaji wa miundombinu ya barabara kuu ya Pwani – Lindi katika eneo la Kimanzichana Kusini lililoathiriwa na mvua na kusababisha barabara hiyo kufungwa kwa muda.
“Niwahakikishie Watanzania hamna haja ya kuwa na wasiwasi pamoja na mvua za El Nino zinazoendelea kunyesha na ikitokea barabara imekatika haitochukua nusu siku kwa namna ambavyo tumejipanga tutakuwa tusharudisha mawasiliano,” amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta, kusimamia kikamilifu Wakandarasi wote waliopewa kazi ya kurejesha miundombinu iliyoathiriwa na mvua kufanya kazi kwa ufanisi na kumaliza ndani ya wakati.
Vilevile, Bashungwa amefafanua kuwa mkakati uliopo ndani ya Serikali ni kurudisha mawasiliano ya muda pindi inapotokea uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja huku Serikali ikisubiria kipindi cha Kiangazi kianze na kufanya matengenezo ya kudumu katika maeneo yote yaliyopata athari.
Bashungwa amelipongeza Jeshi la Polisi na wananchi kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa watalaam wa TANROADS na TARURA wakati inapotokea changamoto yoyote kwenye barabara na kutoa taarifa wakati inapotokea uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa barabara ya Mtwara-Lindi-Pwani-Dar es Salaam kuwa ni barabara ya kiuchumi na kimkakati ambayo inategemewa na wananchi hivyo kupitia TANROADS wameanza kumtafuta mkandarasi atakayeanza kuijenga upya kuanzia Mtwara hadi Mingoyo na baadaye kuendelea kwa awamu mpaka Dar es Salaam.
Pia, Bashungwa ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuanza mchakato wa manunuzi na kumpata Mkandarasi kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya Mbagala Rangi Tatu hadi Vikindu (km 3.8) kuwa njia nne na katikati kutakuwepo na miundombinu ya barabara ya mwendokasi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge ameeleza kuwa TANROADS na TARURA wanaendelea kufanya kazi kubwa kwa ushirikiano wakati zinapotokea dharura katika barabara zote katika Mkoa huo.
Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani, Eng. Baraka Mwambage amesema tayari wamepokea kiasi cha Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya matengenezo ya dharura ya miundombinu ya barabara na madaraja na timu ya wataalamu imejipanga katika maeneo mbalimbali kuendelea kurudisha mawasiliano yaliyopata athari za mvua.