Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amewataka Mameneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuhakikisha wanaendelea kupambana na suala la rushwa katika maeneo yao ya kazi na nje ya kazi ili kujenga taswira nzuri kwa Wakala huo na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha Mamemeja hao, tarehe 17 Novemba, jijini Dodoma, Waziri Bashungwa amesisitiza Mameneja hao kuhakikisha kuwa wanaripoti kwake au katika mamlaka husika endapo watahisi kuna viashiria vyovyote vya rushwa mapema ili hatua stahiki kuchukuliwa kwa wakati.
“Ninyi ni sehemu ya ulinzi katika kusaidia kupambana na rushwa, msisite kuendelea kupambana na suala hili kwa pamoja kuanzia katika hatua za manunuzi hadi kwenye utekelezaji wa mikataba, Mheshimiwa Rais anataka kuona mnafanya weledi mkubwa katika utekelezaji wa miradi, kufanya hivi mtasaidia kulinda rasilimali za serikali zinazopotea kutokana na kukosa uzalendo kwa baadhi ya watu”, amesema Bashungwa.
Aidha, Amewataka Mamemeneja hao kuhakikisha wanachukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa yeyote aliyevamia maeneo ya hifadhi ya barabara na kuendelea kusimamia kwenye maeneo yao kuhakikisha kuwa sheria hiyo haivunjwi.
Waziri Bashungwa amewataka mameneja hao kuwa na tamaduni ya kuwajengea uwezo watumishi wao ili kuongeza ufanisi na tija kwa Taasisi hiyo pamoja na Taifa kwa ujumla samambamba na urithishaji wa ujuzi kwa watumishi walio chini yao kwa lengo la kuwekeza katika vizazi vya sasa na vijavyo .
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewapongeza mameneja hao kwa kazi kubwa wanazofanya katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini na kusisitiza kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa viongozi wa serikali waliopo katika maeneo yao.
” Niwapongeze kwa ushirikiano mnaoutoa kwa viongozi mbalimbali wanapowaita katika mikutano ya kiutendaji au kuwatembelea katika miradi yenu kujua hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi, utaratibu huu ni mzuri nawasihi muendelee nao, hii inaonyesha ni jinsi gani mnaungana nao katika kuhakikisha taarifa za utekelezaji wa miradi zinafahamika kwa wote”, amesema Kasekenya.
Kasekenya amewataka TANROADS kuandaa mkakati wa kuboresha maeneo korofi ambayo yatapewa kipaumbele ili utekelezaji wake uweze kufanyika haraka na kuweza kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Naye, Katibu wa Wizara hiyo, Balozi, Mhandisi Aisha Amour, ameishukuru Wizara ya fedha kwa kuendelea kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 70 kila mwezi kwa ajili ya kulipa madeni ya wakandarasi ambapo kati ya fedha hizo Bil. 20 ni kwa ajili ya wakandarasi wa nje na Bil.50 ni kwa ajili ya wakandarasi wa ndani
” Tunaishukuru serikali kwa juendelea kutugawia kiasi hiki cha fedha ili kupunguza mzigo wa madeni”, tunaamini hali hii ikiendelea madeni ya makandarasi yatakuwa sio changamoto tena”, amesema Balozi Amour.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa Wakala huo, Mtendaji Mkuu wa TANOROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema kuwa Wakala utahakikisha unayafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Waziri huyo ikiwemo kuandaa mpango maalum wa pamoja wa uwekaji wa taa za barabarani katika mikoa yote nchini.
Kikao kazi hicho chenye lengo la kuimarisha ushirikiano na kuboresha utendaji kwa Wakala huo kimeshirikisha viongozi wakuu wa Wizara na Mameneja wa Wakala huo kutoka mikoa yote nchini.