Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah wakipata maelezo kutoka kwa Mhandisi Grace Musita wakati Waziri Mabula alipotembelea ujenzi wa mradi wa nyumba za NHC Kawe jijini Dar es Salaam tarehe 12 Julai 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuangalia namna bora ya kutumia teknolojia ya kisasa katika ujenzi wa nyumba ili kujenga nyumba nyingi na kwa muda mfupi.
Dkt Mabula alisema hayo tarehe 12 Julai 2023 wakati akikagua ujenzi wa mradi wa nyumba unaojulikana kama Samia Housing Scheme unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa kwenye eneo la Kawe jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (katikati) akizungumza na Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah (kulia) pamoja na mhandisi Grace Musita alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa nyumba za NHC Kawe jijini Dar es Salaam tarehe 12 Julai 2023.
‘’Tunahitaji kujenga nyumba siyo tu kwa kutumia matofali tuliyo nayo bali kuwa na teknolojia nyingine itakayotuwezesha ujenzi wa nyumba nyingi na kwa muda mfupi lakini nyumba imara’’ alisema Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Waziri Mabula, nchi zilizoendelea ziko kwenye hatua nzuri kwa kuwa ndani ya mwezi mmoja zinaweza kujenga nyumba ishirini na NHC inatakiwa kupiga hatua kwa kuangalia mabadiliko hayo.
Baadhi ya vibarua wanaofanya kazi katika mradi wa ujenzi wa Nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Hayupo pichani) alipofanya ziara katika mradi huo tarehe 12 Julai 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisisitiza jambo mbele ya Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa nyumba za NHC Kawe jijini jijini Dar es Salaam tarehe 12 Julai 2023.
Hata hivyo, Dkt Mabula alisema, mwaka ujao wa 2024 Tanzania itakuwa mwenyeji wa maonesho ya kimataifa ya tekonolojia ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ambapo Tanzania itaweza kujifunza kutoka kwa wengine.
Aidha, Waziri Mabula alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuliwezesha Shirika la Nyumba la Taifa kukopa fedha za kuendelea na miradi iliyosimama kwa muda mrefu.
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iliruhusu Shirika la NHC kukopa shilingi bilioni 173.9 ambapo hadi sasa Shirika limekopa bilioni 44.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Akielezea zaidi kuhusu uhitaji wa nyumba nchini, Dkt Mabula alisema kuwa, katika sensa iliyopita takwimu zinaonesha upo uhitaji wa zaidi ya nyumba milioni 3.8 na kama ujenzi utafanyika kwa kasi basi zitahitajika kujengwa nyumba laki tano kwa mwaka.
‘’Bado kuna uhitaji mkubwa wa nyumba na sehemu kubwa ya nyumba zinazojengwa na Shirika letu la NHC watu wameonesha nia ya kuzichukua na kwa mujibu wa sensa iliyopita upo uhitaji mkubwa wa nyumba katika jiji la Dare es Salaam’’ alisema Dkt Mabula
Hata hivyo, alisema, habari njema ni kuwa, kupitia Bajeti ya 2023/2024 wananchi sasa wanaoenda kununua nyumba za gharama nafuu wameondolewa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) hivyo nyumba ya milioni 50 kushuka chini itanunuliwa bila VAT.
Kufuatia hatua hiyo, Dkt Mabula aliweka bayana kuwa, inachofanya serikali ni kuhakikisha nyumba za aina hiyo zinajengwa kwa wingi ili watanzania waweze kununua. Ametoa rai kwa watu wenye fursa ya kuendeleza ujenzi kufanya hivyo kwa kuwa uhitaji wa nyumba bado ni mkubwa.
Shirika la Nyumba na Taifa (NHC) lilibuni mradi wa nyumba 5000 za gharama nafuu wa Samia Housing Scheme zitakazojengwa kwa awamu katika mikoa mbali mbali nchini kwa gharama ya shilingi bilioni 466. Kwa kuanzia, Shirika lilianzisha ujenzi wa nyumba 560 Kawe Jijini Dar es Salaam.
1 Comment
ラブドール セックス2019,page 183.