Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kutenga Shilingi milioni 50 kutoka mapato yake ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Mwamayoka, akisisitiza kuwa wananchi hawapaswi kuendelea kuteseka kwa kukosa huduma za afya.

Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Upanuzi wa Mtandao wa Majisafi ya Ziwa Victoria kutoka Makomero – Mgongoro, Majaliwa amesema kuwa halmashauri hiyo imekusanya zaidi ya Shilingi bilioni 4, lakini bado inasubiri fedha kutoka Serikali Kuu kwa miradi midogo kama ujenzi wa zahanati.
“Halmashauri hii mmekusanya mpaka sasa zaidi ya bilioni 4, lakini bado mnategemea pesa kutoka Serikali Kuu kwa kila jambo? Zahanati ya Shilingi milioni 50 mnasubiri bajeti ijayo? Hapana, tumieni pesa mliyonayo sasa kujenga zahanati hii,” amesisitiza Majaliwa.

Ameagiza Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga kuhakikisha ifikapo Aprili 2025, fedha hizo zinatolewa na ujenzi wa zahanati unaanza mara moja.
“Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, leta Shilingi milioni 50 kwa ajili ya zahanati hii. Wananchi hawa wanateseka kutafuta huduma za afya mbali, hali ambayo haikubaliki. Kama wananchi wameshaanza ujenzi, basi fedha hizi zitumike kumalizia,” ameongeza.
Aidha, Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora kusimamia utekelezaji wa agizo hilo, akisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma za msingi za afya zinapatikana karibu na wananchi bila usumbufu.

Hii ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya afya vijijini, kwa kuhakikisha kuwa kila kijiji kinakuwa na angalau zahanati yenye vifaa na watumishi wa kutosha ili kupunguza mzigo kwa hospitali za wilaya na mikoa.