Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amemsifu Mbunge wa Jimbo la Itilima, Njalu Daudi Silanga, kwa ubunifu na juhudi zake katika kuwaletea wananchi maendeleo, akisema kuwa mchango wake umeleta mabadiliko makubwa katika wilaya hiyo.

Akizungumza katika Uwanja wa Stendi uliopo katika kata ya Lagangabilili wilayani Itilima mkoani Simiyu siku ya Jumamosi Februari 15, 2025 katika Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Itilima, Waziri Mkuu amesema kuwa mafanikio mengi yaliyopatikana katika wilaya hiyo yamechangiwa na ubunifu na ufuatiliaji wa karibu wa Mbunge Silanga.
“Ninataka nimpongeze mbunge wenu. Mambo mengi mazuri yanayofanyika hapa yanahitaji ubunifu wa mtu, na Mheshimiwa Silanga ni mbunifu wa kweli. Muda mwingi anakaa jimboni, anafuatilia miradi, anatembelea wananchi wake, na amefanikisha maendeleo makubwa. Hakika huyu ni mbunge bora kabisa,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Majaliwa ameendelea kueleza kuwa wananchi wa Itilima wamempatia Silanga jina la “Profesa wa Maendeleo” kutokana na juhudi zake za kuhakikisha wilaya inasonga mbele kimaendeleo.

“Huyu anayo sifa inayosababisha yeye kuitwa profesa, lakini kwa namna anavyojituma, kufikiria na kuumiza kichwa kuhakikisha Itilima inakua, ni kweli ni profesa wa maendeleo,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa pongezi kwa Mkuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, na watumishi wa Serikali kwa kushirikiana na mbunge katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa weledi na kuhakikisha kila shilingi inawanufaisha wananchi.
“Tunapojivunia mafanikio haya, hatuwezi kuacha kuwapongeza watumishi wa halmashauri ambao wamesimamia fedha na miradi kwa uadilifu. Mafanikio haya ni matokeo ya mshikamano kati ya Serikali, wananchi, na chama, ambapo wote mnazungumza lugha moja ya maendeleo,” ameongeza Majaliwa.

Mkutano huo ulilenga kuwasilisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020/25 jimboni Itilima.
2 Comments
I appreciate your ability to break down complex ideas into digestible segments. Well done!
Reading your blog posts feels like attending a valuable class.