Uncategorized KITAIFA BIASHARA

WAZIRI ULEGA AAGIZA KUPUMZISHWA KWA MIEZI MITATU SHUGHULI ZA UVUVI ZIWA TANGANYIKA, ATUMBUA MMOJA

WAZIRI ULEGA AAGIZA KUPUMZISHWA KWA MIEZI MITATU SHUGHULI ZA UVUVI ZIWA TANGANYIKA, ATUMBUA MMOJA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ametangaza mpango wa Serikali wa kupumzisha  shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu ili kuwezesha samaki kuzaliana na kuongeza tija kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao ziwani humo.
 
Waziri Ulega  ametoa kauli ya serikali kwa nyakati tofauti ambapo awali alitoa kauli hiyo akizungumza na wadau wa uvuvi kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma na baadaye kuzungumza na wananchi na wadau wanaofanya shughuli za uvuvi kwenye Mwalo wa Katonga Manispaa ya Kigoma Januari 9, 2023.
 
Akiwa kwenye kikao cha ndani na wadau wa uvuvi Waziri Ulega alisema kuwa utekelezaji wa mpango huo utaanza rasmi Mei 15 hadi Agosti 15 mwaka huu na hiyo ikiwa ni Utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika unaoweka hatua na taratibu za usimamizi endelevu wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.
 
“Pamoja na kufunga shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika, Serikali ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza kutekeleza njia mbadala za kuwawezesha wananchi kujiendeleza kiuchumi katika ziwa Tanganyika ikiwemo kukopesha vikundi maboti na vizimba kwa ajili ya miradi ya ufugaji wa samaki na tayari imetenga shilingi milioni 200 kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kubainisha maeneo yanayofaa kwa ufugaji huo,’ alisema Waziri Ulega

Aliongeza kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia ametoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha uzalishaji wa vifaranga vya samaki bora mkoani humo kwa ajili ya kuwawezesha wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kuwa na uhakika wa kupata vifaranga bora wakati wote.

Wabunge wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Kilumbe Ng’enda wa Kigoma Mjini na Mhe. Josephine Genzabuke wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Waziri Ulega uliofanyika katika mwalo wa Katonga wameunga mkono mpango huo wa serikali na kusema utaleta faida kubwa kwa sekta ya uvuvi.

ULEGA AMSIMAMISHA KAZI AFISA MFAWIDHI KIGOMA

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Agnes Meena kumsimamisha kazi Afisa Mfawidhi anayeshughulikia ubora wa samaki kituo cha Kigoma, Bw. Frank Kabitina kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.

Waziri Ulega ametoa maelekezo hayo alipokuwa akizungumza na wananchi katika Mwalo wa Katonga Mkoani Kigoma Januari 9, 2024.

Alisema Afisa huyo amekuwa akikusanya mapato ya mazao ya uvuvi na sehemu ya mapato hayo akiyatumia kwa manufaa yake binafsi.

“Naibu Katibu Mkuu, Afisa huyu hakuna haja ya kusema achunguzwe, mtoe kwanza wakati mtakapokuwa mnaendelea kumchunguza na atakayekuja mtahadharisheni, tunataka mtu muadilifu”, alisema

About Author

Bongo News

1 Comment

    Your article helped me a lot, is there any more related content? Thanks!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *