KITAIFA

WAZIRI UMMY AZINDUA MPANGO KABAMBE WA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA, IRINGA

WAZIRI UMMY AZINDUA MPANGO KABAMBE WA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA, IRINGA

Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya huduma za afya nchini, upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa, na kuongeza wataalamu wa sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya nchini

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango kabambe wa kambi ya ‘Madaktari Bingwa’ wa Rais Samia unaolenga kufikia Hospitali zote 184 za Halmashauri nchini, hafla iliyofanyika kwenye viunga vya Hospitali ya Manispaa ya Iringa (Frelimo) kitaifa leo, Jumatatu Mei 06.2024 ambapo amesema mpango huo unalenga kutimiza dhamira na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan unaokusudia kuona Watanzania wanapata huduma bora za afya nchini

Waziri Ummy amesema mpango huo unalenga kubadilishana ujuzi, na uzoefu baina ya ‘Madaktari Bingwa’ wa Rais Samia na Madaktari wanaowakuta kwenye Hospitali za wilaya lengo likiwa ni kuhakikisha baada ya Madaktari hao kuondoka waache alama ya kufanyika kwa zoezi endelevu kwenye sekta hiyo

Sambamba na hilo amesema mpango huo unalenga kusaidia Hospitali za wilaya kuanzisha, na kusaidia uanzishwaji wa wodi maalumu za watoto wachanga (siku 0 hadi 28), kuanzisha vifaa visaidizi vya kusaidia watoto wachanga kupumua jambo ambalo ameagiza Halmashauri mbalimbali nchini kufanikisha ununuzi wa vifaa hivyo ili kwa pamoja kusaidia kuokoa maisha ya watoto wachanga pale wanapopata matatizo hayo

Amesema serikali ya awamu ya sita (6) inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanikisha kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa zaidi ya asilimia 80 lakini, bado kuna changamoto kwenye vifo vya watoto wachanga kwa kuwa vimepungua kwa asilimia nne (4) pekee hivyo ni wakati muafaka sasa kila mmoja kwa nafasi yake kuunga mkono juhudi za Rais Samia kuhakikisha vifo vya watoto wachanga vinapungua kwa kiasi kikubwa, kwa kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema uwepo wa wodi maalumu ya watoto wachanga unapunguza vifo hivyo kwa zaidi ya asilimia 50

Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa viongozi mbalimbali wa serikali ngazi za mikoa, wilaya na Halmashauri kote nchini kufanya kazi kwa karibu na Madaktari hao, sambamba kuwahamasisha wananchi kufika kwenye Hospitali hizo kwa ajili ya kuonana na Madaktari hao ambao watatumia siku tano (5) kuwepo kwenye Hospitali moja

Kwa mujibu wa Waziri Ummy amesema Madaktari hao ni pamoja na Madaktari Bingwa wa magonjwa ya afya ya uzazi, Madaktari Bingwa wa watoto na watoto wachanga, Madaktari Bingwa wa upasuaji, Madaktari Bingwa wa magonjwa ya ndani na Madaktari Bingwa wa huduma za ganzi na usingizi

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Iringa, Mkuu wa wilaya ya Iringa Kheri James ameishukuru serikali ya awamu ya sita (6) inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa iliyofanya mkoani humo kwenye sekta ya afya ndani ya muda mfupi ambapo mageuzi hayo yanahusisha uboreshaji wa miundombinu kwenye maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za afya, ununuzi wa vifaa na vifaa tiba vya kisasa nk

Hata hivyo kupitia hadhara hiyo Kheri James ameomba Hospitali hiyo ijengewe jengo maalumu la OPD, sambamba na kupatiwa gari litakalotumiwa na Mganga Mkuu wa wilaya hiyo (DMO) kwenye shughuli zake za kila siku

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI, viongozi wa serikali ngazi ya mkoa, wilaya na Halmashauri za mkoa wa Iringa, viongozi wa CCM na wananchi wa Iringa kwa ujumla wake.

About Author

Bongo News

5 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *