Waziri wa elimu nchini Tanzania Prof. Adolf Mkenda leo Machi 18, 2025 amekaribisha wafadhili mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, kufadhili masomo ya ufundi na ufundi stadi kwa vijana wa Kitanzania kama ambavyo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na baadhi ya Taasisi za kifedha zimekuwa zikifanya.

Prof. Mkenda amebainisha hayo wakati akitoa salamu zake fupi kwenye maadhimisho ya miaka 30 ya VETA, akisema serikali pia imetoa ruzuku kubwa kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya ufundi stadi kwa kuweka ada ya shilingi 120,000 kwa wanafunzi wa bweni na Shilingi 60,000 kwa wanafunzi wanaotokea nyumbani.
Aidha Waziri Mkenda pia ameahidi kuwa kama wizara msisitizo mkubwa sasa umekuwa ni kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya kujenga vyuo vya ufundi stadi kwenye wilaya zote nchini ili kuhakikisha fursa zaidi kwa vijana wanaopenda kuwa na ujuzi na stadi mbalimbali za maisha.

Amemshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kuendelea kuiunga mkono wizara na Taasisi ya VETA, Akisema katika maadhimisho ya miaka 30 ya Taasisi hiyo shughuli mbalimbali zinafanyika nchi nzima ikiwemo upakaji wa rangi kwenye jengo la watoto la Hospitali ya Taifa Muhimbili na kwenye majengo ya taasisi mbalimbali za serikali.