Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman amewasihi wananchi wa Kaskazini Unguja Visiwani Zanzibar, kujitokeza kwa wingi kwenye siku tisa za utekelezaji wa kampeni ya msaada wa Kisheria kwenye Mkoa huo, akimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu na ufadhili wa kampeni hiyo, aliyoitaja kuwa muhimu kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kiuchumi.

Mhe. Haroun ambaye amekuwa Mgeni rasmi katika uzinduzi huo leo Jumatano Aprili 23, 2025, kwenye Uwanja wa Tumaini Skuli ya Mkwajuni Kaskazini Unguja, akieleza matarajio yake kuwa Kampeni hiyo itaondoa misururu mirefu ya wananchi wanaofuata majawabu ya Changamoto zao mbalimbali za kisheria kwenye Ofisi za wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Masheha kwa upande huo wa Zanzibar.

“Wanyonge walikuwa hawana uwezo na tunawajua, wanapata shida sana wanapodai haki zao, sasa muarobaini umepatikana. Kuna matatizo mengi mnayo, matatizo ya ardhi, lakini hata wafanyakazi mnaofanya kazi katika mahoteli na maeneo mengine mnahitaji msaada wa kisheria kwani pengine kuna haki zao nyingi wanazikosa, wanafanyishwa kazi kinyume na taratibu, sasa hii ni fursa muhimu kuhakikisha mambo hayo tunayapunguza ama tunayamaliza kabisa.” Amesema Mhe. Waziri.

Akisisitiza kuwa matatizo mengi na migogoro ya kijamii inasababishwa na Uvunjifu wa sheria unaofanywa na baadhi ya watu, Mhe. Haroun amemshukuru pia Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania bara, Mhe. Damas Ndumbaro kwa namna Wizara yake imekuwa ikishirikiana na Wizara yake katika masuala mbalimbali, akiomba Ushirikiano huo uendelee na ufanyike kwenye Wizara nyingine, kama sehemu ya kusaidia ustawi wa wananchi wa pande mbili hizi za muungano suala ambalo litaimarisha pia muungano.

Katika hatua nyingine, Mhe. Haroun amewahimiza wananchi wa Zanzibar na Tanzania bara kuendelea kuilinda na kuitunza amani ya Tanzania kuelekea uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu, akieleza kuwa upatikanaji wa haki umeegemea zaidi katika amani na utulivu kwani kukosekana kwake, Haki hukandamizwa na sauti za wananchi kutosikika kwenye vurugu.

About Author

Bongo News

18 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *